Songea ni jina la mji maarufu zaidi kusini magharibi mwa Tanzania katika mkoa wa Ruvuma. Mji huu unakadiriwa kuwa na watu wapatao laki tatu na ni makao makuu ya mkoa wa Ruvuma na pia jimbo kuu la Kanisa katoliki la Songea.
Mji huu mkongwe ulipata sifa kubwa kutokana na wakazi wake kuwa mstari wa mbele katika kupambana na ukoloni na hasa katika vuguvugu la Majimaji dhidi ya wakoloni wa Kijerumani.
Jina la Songea limerithishwa kutoka kwa Chifu wa kabila la Wangoni Nduna Songea Mbano aliyenyongwa na wajerumani mwaka 1906 kwa kukataa utawala wa kikoloni.
Mji wa Songea unaunganishwa na barabara kubwa tatu za lami yaani ile ya kutokea Iringa na Njombe, ya Mtwara na Masasi na ya tatu ni ile iendayo Mbinga hadi Mbambabay huko ziwa Nyasa. Mji huu una kiwanja cha ndege kinachopanuliwa hivi sasa ili kuweza kutua ndege kubwa. Uwanja huo wa ndege upo eneo la Ruhuwiko ambako pia kinapatikana chuo cha Mt. Thomas yaani STIMAT.
Songea inatambulika kwa hali ya hewa ya kadiri na isiyokera na hivyo kuufanya kuwa mkoa unaoongoza kwa uzalishaji wa chakula.
Mji wa Songea ni maarufu kwa michezo na burudani mbalimbali na kwa miongo kadhaa timu yake ya mpira wa miguu (Majimaji FC) ilishiriki ligi kuu n ahata kuwa bingwa wake kwa miaka kadhaa. Pia kuna tamasha maarufu la Utamaduni liitwalo “Majimaji Selebuka” linalohusisha maonyesho ya Utamaduni na Mbio za Marathoni na Baiskeli.
Kwa ufupi Songea ni Zaidi ya mji wa kiTanzania unaokupa kila utakacho kwa ubora na gharama nafuu,
Karibu Songea!